Sunday, December 18, 2016

BREAKING NEWS!!

Diwani wa Chadema Kata ya Boma Jimbo la Mafinga Mjini ndugu Kisoma amesimamishwa  Udiwani na Tume ya Uchaguzi ya Taifa baada ya kuthibitika hajui kusoma na kuandika.

Friday, December 16, 2016

SERIKALI IMEJIPANGA KUHAKIKISHA SEKTA YA KILIMO INATOA MCHANGO KATIKA KUFIKIA NCHI YENYE UCHUMI WA VIWANDA

Na.Immaculate Makilika.

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imesema kuwa imeandaa mikakati mbalimbali  ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo  inatoa mchango zaidi katika kufikia nchi ya uchumi wa kati.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa na kituo cha televisheni cha TBC, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye sasa ni Katibu Mkuu  Wizara ya Ulinzi Dkt. Florence Turuka alisema kuwa Serikali imeandaa mikakati hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili viwanda viweze kupata malighafi, chakula cha kutosha pamoja na ajira kwa wananchi.

“Serikali imeamua kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mazao kwa ajili ya soko, kushirikisha sekta binafsi katika kuongeza thamani ya mazao, ili kuvutia wakekezaji katika sekta ya kilimo  nchini” alisema Dkt. Turuka.

Kwa mujibu wa Dkt. Turuka alisema ili kuhakikisha huduma za ugani zinakua za kisasa   Serikali inadhamiria kutumia simu za mkononi zitakazorahisisha utoaji wa  taarifa kwa wataalamu wa kilimo, ikiwa ni pamoja na kusaidia wakulima kupata huduma za kitaalamu kwa wakati.

Aidha Dkt. Turuka alisema mikakati mingine inayotekelezwa na  Serikali ni pamoja na kuongeza idadi ya  matrekta hadi kufikia 6,000 badala ya 400 yaliyokuwepo awali.
Aliongeza kuwa Serikali imekusudia pia kujenga maghala karibu na maeneo yanayozalisha mazao ya matunda na mbogamboga ili kuweza kuyahifadhi kwa muda kabla mazao hayo hayajapekelekwa sokoni ili kupunguza uharibifu.

Naye Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mathew Mtigumwe alisema Serikali itaboresha mfumo wa takwimu wa wataalamu wa kilimo pamoja na kuwajengea uwezo ili kusaidia utekelezaji wa maendeleo ya kilimo katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Serikali inawakaribisha wawekezaji wa kilimo cha miwa ambapo imeandaa zaidi ya hekta 6000 kwa ajili ya kilimo hicho nchini.

WATAYARISHAJI FILAMU WATAKIWA KUWA WABUNIFU.

Na. Genofeva Matemu.

Watayarishaji wa kazi za ubunifu ikiwemo filamu Tanzania wamehaswa kuwa wabunifu na kuacha kunakili kazi ambazo zilishafanywa na watu wengine kwani kwa kufanya hivyo hupelekea kudidimiza sekta ya Filamu na kuidhalilisha tasnia ya uigizaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bw. Ado Mapunda alipokua akifunga warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza iliyofanyika kwa siku tatu na kufungwa leo Mkoani Mara.

“Tumieni fursa hii ya kipekee kuchota maarifa ya kutosha yatakayowaongezea ujuzi katika kazi zenu za filamu. Naamini baada ya warsha hii mtalenga kutoa kazi bora zitakazokidhi mahitaji ya wadau wenu na pia zitakazoweza kushindana kwenye soko la ndani na kimataifa” amesema Bw. Mapunda

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao ameiomba Ofisi ya Mkoa wa Mara na Wilaya zake kushirikiana na kuhimiza Sekta ya Utamaduni kutengewa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Filamu huku wakijumuishwa katika fursa mbalimbali ikiwepo mikopo kupitia mfuko wa vijana na wanawake ambapo itasaidia vijana na wanawake  wengi ambao wanajishughulisha na Tasnia ya filamu Kwa kuwa filamu inaweza kuchangia ustawi wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na pia kuchangia pato la nchi kwa kiwango kikubwa.

Naye katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo amewaomba watayarishaji wa kazi za filamu kuwasilisha miswada yao kabla ya kuandaa filamu zao ili bodi ya filamu ipate fursa ya kupitia miswada hiyo na kuiboresha kabla ya filamu kuandaliwa jambo ambalo litasaidia kuondokana na filamu zitakazokua zinazuiliwa kutokana na makosa madogo madogo yanayojitokeza katika filamu zao.

Aidha watayarishaji wa Mkoa wa Mara wametakiwa kutumia maarifa ya warsha hiyo kutengeneza filamu zinazohamasisha uwajibikaji, umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, athari za ukeketaji, athari za uvuvi haramu kama baadhi ya maeneo ambayo jamii ya Mkoa wa Mara inahitaji kuelimisha na kuondokana na dhana potofu.

Mafunzo hayo yameshirikisha zaidi ya wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza 200 kutoka Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Manispaa ya Mosoma, Musoma Vijijini, Bunda Mji, Tarime Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Lorya, Butihama na wadau kutoka Mkoa jirani wa Simiyu.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa waadilifu  wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za kisheria walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.
Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.

MWILI WA BRIGEDIA JENERALI MHAIKI WAAGWA RASMI LEO.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akifuatana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt.Hussein Ali Mwinyi  (kushoto) na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange (kulia)wakati Rais alipofika leo katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo Dar es Salaam kwa ajili ya kuuaga mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi hospitalini hapo baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitia saini kitabu cha kumbukumbu ya Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki, aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,ambae alifariki juzi katika  hospitali  ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo JIjini Dar es Salaam,baada ya kuugua kwa muda mfupi na kuagwa leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt.Hussein Ali Mwinyi  (kushoto) na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange (kulia) wakiwa katika Kambi ya Jeshi la Wananchi Lugalo Dar es Salaam leo   kuuaga mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Baadhi ya Maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ waliofika leo katika hafla ya kuuaga Mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo, baada ya kuugua kwa muda mfupi,ambapo utaagwa leo katika Hospitali Lugalo Dar es Salaam.

Wananchi mbali mbali na jamaa waliofika leo   kuuagawa  Mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Jeneeza lenye Mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki  aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali  ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo   Dar es Salaam,ukibebwa  na askari kupelekwa sehemu maalum ambapo utaagwa rasmi leo kabla kupelekwa kijijini kwao kwa mazishi.

Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Viongozi pamoja na Wazee wa Chama leo walijumuika na Maaskari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kuuaga Mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa heshima ya mwisho leo kwa mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki aliyekua Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar,aliyefariki juzi katika hospitali ya Jeshi la Wananchi JWTZ Lugalo Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mfupi.


JPM APONGEZWE URATIBU MAAFA KAGERA.

Na. Joseph Martin, Nottingham  
WATANZANIA bado tuko katika masikitiko kufuatia maafa yaliyoletwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera na baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa. Tetemeko hilo tunaambiwa ni la kiwango cha skeli ya 5.7 ambayo ni kubwa.

Watu 17 wamefariki kutokana na tetemeko hilo, mamia wamejeruhiwa na maelfu ya nyumba ama zimebomoka au zimeharibika kwa namna tofauti. Mimi binafsi nina ndugu zangu ambao ni waathirika wa tukio hili na namshukuru Mungu kwa misaa waliyopata.

Nimefuatilia sana yanayotokea kule Kagera na naendelea kufuatilia kwa sababu jamaa zetu wa kule kwa kweli wanahitaji msaada wetu ingawa na wao pia wanapaswa kuchukua hatua zao na za jamaa zao wa karibu katika kujinasua na janga lililowafika.

Maoni yangu leo si ya kueleza tukio hilo wala kufafanua maafa yalivyowagusa ndugu, jamaa na marafiki zetu, bali kimsingi, nimeandika kufikisha ujumbe kwa Mhe Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli. Nitaeleza kwa nini Dkt. Magufuli anapaswa kupewa hongera zake katika hili.

Mosi, tufahamu kuwa hili ni janga  la asili na ni jambo ambalo wanasayansi wanasema halitabiriki na hakuna mtu anaweza kujua lini tetemeko la ardhi litatokea. Lakini hata tukijua, bado ni ngumu kuzuia athari zake hasa kwa makazi na miundombinu.

Lakini tangu kutokea kwa jambo hili, labda tofauti na ilivyopata kutokea katika majanga mengine nchini kama vile mafuriko ya Kilosa na majanga mengine ya tetemeko au mafuriko, kwa mara ya kwanza, na ikiwa haina uzoefu bado wa muda mrefu katika uongozi, Serikali ya Magufuli imetuunganisha na imetutendea haki sana kwa kiwango chake.

Mara tu baada ya tukio, Waziri Mkuu alifika Kagera kuwajulia hali waathirika, kushiriki mazishi ya umma ya waliofariki na kutoa maagizo kwa watendaji wake juu ya hatua za haraka za kufanywa.

Mara tu baada ya Waziri Mkuu kutoka Kagera, Rais Magufuli ambaye hata baadhi ya watendaji wake waandamizi walishakuwa mjini Lusaka, Zambia alikokuwa aende kwa ajili ya sherehe za kuapishwa Rais Lungu, naye aliahirisha safari hiyo.

Rais aliahirisha safari na kubaki Dar es Salaam kuratibu kwa karibu maafa hayo na namna ya kuwasaidia waathirika. Na mara moja tuliona athari za uwepo wake nchini ambapo ilifanyika harambee Ikulu ambapo watanzania tukahamasishwa kuchangia.

Serikali ikachukua hatua muhimu za mawasiliano na hamasa kwa wadau ikiwemo kutangaza akaunti ya maafa na namba za simu za sisi kuchangia. Akaunti hizi, tofauti na miaka ya nyuma zimesambazwa sana katika mitandao ya kijamii na hata nimeona matangazo katika magazeti na katika televisheni. Mkuu wa Mkoa wa Kagera anatoa taarifa za mara kwa mara pia.

Serikali pia kupitia taasisi na wizara mbalimbali pia imeendesha matukio mengine ya kuchangia waathirika, imeratibu nchi nyingine za kigeni na Balozi kupeleka misaada Kagera na misaasa hiyo imeanza kuwafikia waathirika.

Nafahamu kuwa Serikali haikuwa na wajibu wa moja kwa moja katika hili kwa kuwa haikusababisha, lakini juhudi hizi ni za kupongezwa sana na za kukumbukwa sana. Mzee Magufuli Mungu akutangulie.

Nnitumie fursa hii pia kuwasihi watanzania wenzangu, katika kuwasaidia wenzetu, kama tulivyoanza, kusiwe tena na siasa wala watu kutafuta upungufu na kukosoa. Kila mmoja wetu “ajiongeze” wanasema vijana wa  mjini.

Hata kwa ndugu zangu waathirika nao pia tujue sisi na jamaa zetu tuna jukumu la kwanza katika hili na tujitume kujinasua katika janga hilo, Serikali inaweza kuleta kidogo cha kuchangia au kutufuta machozi, au kurekebisha miundombinu ya umma lakini tusibaki watu wa kusubiri tukidhani ndio tutafanyiwa kila kitu.

Hakuna Serikalini duniani inayoweza kufanya kila kitu hasa yanapotokea majanga makubwa hata ziwe na uwezo vipi. Niliwahi kufika Marekani kwenye eneo la janga la Septemba 11 pale Manhttan, New York na kukuta hata baada ya miaka 10 eneo lile halikuwa limeweza kurejea katika hali yake ya awali.

Kuna eneo kule Japan baada ya maafa ya mafuriko nimepata kuvikuta vikiwa hadi leo haviko katika sura yake ya awali. Naamini hata ndugu zangu wa Kagera wajue hili, yapo mambo yanaweza kufanyika yakawa bora zaidi kwa jitihada zao na za Serikali, lakini pia yapo yanayoweza kuchukua muda zaidi na au hata yasirejee katika hatua kama za awali.

Nihitimishe, hongera kwa JPM lakini pia Serikali na wadau wengine tuendeleze moyo huu huu na ushirikiano huu huu katika matukio mengine mengi zaidi yawe ya maafa au ya kawaida. Kama tulivyoungana katika suala la madawati na hili la maafa, naamini tukiendelea kuungana pamoja, Tanzania itasonga mbele.

Nawashukuru sana.