Friday, December 16, 2016

WATAYARISHAJI FILAMU WATAKIWA KUWA WABUNIFU.

Na. Genofeva Matemu.

Watayarishaji wa kazi za ubunifu ikiwemo filamu Tanzania wamehaswa kuwa wabunifu na kuacha kunakili kazi ambazo zilishafanywa na watu wengine kwani kwa kufanya hivyo hupelekea kudidimiza sekta ya Filamu na kuidhalilisha tasnia ya uigizaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bw. Ado Mapunda alipokua akifunga warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza iliyofanyika kwa siku tatu na kufungwa leo Mkoani Mara.

“Tumieni fursa hii ya kipekee kuchota maarifa ya kutosha yatakayowaongezea ujuzi katika kazi zenu za filamu. Naamini baada ya warsha hii mtalenga kutoa kazi bora zitakazokidhi mahitaji ya wadau wenu na pia zitakazoweza kushindana kwenye soko la ndani na kimataifa” amesema Bw. Mapunda

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao ameiomba Ofisi ya Mkoa wa Mara na Wilaya zake kushirikiana na kuhimiza Sekta ya Utamaduni kutengewa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Filamu huku wakijumuishwa katika fursa mbalimbali ikiwepo mikopo kupitia mfuko wa vijana na wanawake ambapo itasaidia vijana na wanawake  wengi ambao wanajishughulisha na Tasnia ya filamu Kwa kuwa filamu inaweza kuchangia ustawi wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na pia kuchangia pato la nchi kwa kiwango kikubwa.

Naye katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo amewaomba watayarishaji wa kazi za filamu kuwasilisha miswada yao kabla ya kuandaa filamu zao ili bodi ya filamu ipate fursa ya kupitia miswada hiyo na kuiboresha kabla ya filamu kuandaliwa jambo ambalo litasaidia kuondokana na filamu zitakazokua zinazuiliwa kutokana na makosa madogo madogo yanayojitokeza katika filamu zao.

Aidha watayarishaji wa Mkoa wa Mara wametakiwa kutumia maarifa ya warsha hiyo kutengeneza filamu zinazohamasisha uwajibikaji, umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, athari za ukeketaji, athari za uvuvi haramu kama baadhi ya maeneo ambayo jamii ya Mkoa wa Mara inahitaji kuelimisha na kuondokana na dhana potofu.

Mafunzo hayo yameshirikisha zaidi ya wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza 200 kutoka Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Manispaa ya Mosoma, Musoma Vijijini, Bunda Mji, Tarime Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Lorya, Butihama na wadau kutoka Mkoa jirani wa Simiyu.

No comments:

Post a Comment