WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka
na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na
kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa
kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati akihutubia wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri
Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa
waadilifu wanamega kiwanja cha shule na
kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa
taarifa ya hatua za kisheria walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu
wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja
hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza
viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha,
Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na
Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa
agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na
kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema
Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya
kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi
na shughuli zingine za kijamii.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw.
Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya
na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa
hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.
Akizungumzia
kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika
la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.
Naye
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro
Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro
huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro
inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya
Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa kinyemela
na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema
baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani
Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi
mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.
No comments:
Post a Comment