Na. Joseph Sabinus, Nottingham University
JUZI niliandika makala
kuonesha kuwa kelele zinazoendelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari
ukizitazama kwa undani utakubaliana nami kuwa ni matokeo ya kada isiyojiamini.
Tasnia ya habari hapo
nchini haijiamini na hili linaweza kuelezwa ama na miaka mingi ya kuhangaika
kuwa na sheria yao huku zoezi hilo kila mara likikumbwa na sababu mbalimbali na
kuahirishwa au kwa namna wanavyojenga hoja zao.
Hata hivyo ukiziacha kelele
hizo na kuanza kuusoma muswada huu kwa kina na kwa kutafakari makosa mengi
yanayofanywa na vyombo vya habari popote duniani utakubaliana nami kuwa muswada
huu, kama walivyosema pia Tanganyika Law Society na Twaweza, una mambo mengi
mazuri na ni bora zaidi kuliko ile ya awali.
Nilidhani wanahabari
wangeshiriki vyema katika kuboresha yale maeneo yenye changamoto badala ya
kuwaachia watu wa tasnia nyingine. Ni bahati mbaya wadau hawa wamechagua kuwa
wanaharakati zaidi badala ya wanataaluma.
Binafsi baada ya kuusoma
muswada nimebaini masuala makubwa yafuatayo katika hili. Naomba tushirikiane.
1.
Sheria kutosajili mitandao
Awali nilipomsoma
Mbunge Zitto Kabwe nilistushwa kusikia kuwa sheria hii inalenga kubana hadi
mitandao ya kijamii. Hata hivyo sheria haisomwi kama gazeti.
Wakati Zitto alikuwa
akisoma tafsiri ya neno “media” na kuona limejumuisha mpaka mitandao ya
kijamii, ukweli ni kwamba ukiusoma muswada ule eneo ambalo sheria itahusika
nalo kwa maana ya uratibu ni sekta iitwayo “print media”
Kwa hiyo ni
kujidanganya kusema sheria hii itasajili mitandao ya kijamii na vitu
vinavyofanana na hivyo. Badala yake ukisoma kifungu cha 8(1) unauona ukweli
huu. Mitandao imekuwa kama chombo kingine cha habari lakini nadhani kuanza kuisajili sasa ni mapema mno.
2.
Habari ni
taaluma
Kwangu
mimi, sijui kwa wanahabari wenyewe, muswada huu unaleta kwa mara ya kwanza
mfumo madhubuti wa kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma kamili na
itakayoheshimika na kutambuliwa zaidi.
Ukiutazama
mfumo unaopendekezwa wa Bodi ya Ithibati katika ibara ya 10 utaiona “spirit”
hii. Taaluma kuwa taaluma moja ya sifa ni hii. Lazima wanataaluma hiyo wawe na
Bodi inayowasajili kwa viwango vilivyowekwa. Hata hivyo sijapata sababu kwa
nini sifa hazijaanishwa kwa sasa.
3.
Bodi
kumilikiwa na wanahabari
Wakati nikiendelea
kuusoma muswada huu pia nilipatwa na wasiwasi kuhusu kuundwa kwa Bodi hiyo ya
Ithibati nikidhani ingejaa warasimu tunaowafahamu siku zote.
Hata hivyo kama kuna
jambo lingine la kuusifu muswada huu ni pamoja na muundo wa Bodi yake. Bodi
itakuwa na wajumbe 7 na kati ya hao wanne (4) watakuwa ni wanataaluma ya habari
akiwemo mwenyekiti wa Bodi.
Haya ni mapinduzi
makubwa katika uundaji wa Bodi za kitaaluma ambapo katika maeneo mengine
ingezingatiwa tu uwakilishi labda wa jinsi, umri au taasisi. Katika hili
tuwapongeze waliosanifu muundo wa Bodi hii.
4.
Bara Huru
lenye meno
Hapa nianze kwa
kusema muswada huu umechelewa sana na hakuna hoja wala haja ya kusubiri tena.
Wananchi wanahitaji kuhudumiwa na sekta bora zaidi ya habari na kila mmoja wetu
anajua umuhimu huu.
Ukisoma kifungu cha
23 na kuangalia majukumu yale ya Baraza Huru la Habari utakubaliana nami kuwa
tunahitaji Baraza hili Huru kuliko wakati wowote. Hilo Baraza linalotajwa
kuwepo ni NGO tu na Serikali yoyote duniani haiwezi kuendeshwa na NGO.
Baraza linaloundwa
humu nimeona litakuwa na uhuru na haki ya kutunga kanuni za maadili za
wanahabari na kuhakikisha wenyewe wanazielewa katika kuwasimamia kwenye kazi
zao. Hii ni muhimu sana.
Ukienda Mahakamani
inachukua miaka. Ukienda MCT ya sasa hata wakitoa uamuzi chombo cha habari
kinakuwa na uhuru wa kuukataa au kuukubali uamuzi huo. Baraza hili kwa kuwa
limeanzishwa kisheria na lina nguvu za kisheria litakuwa na uwezo wa kusimamia
hata utekelezaji wa hukumu zake.
5.
Wanahabari
kutunga kanuni zao
Katika
hili niseme tu kwamba kama kuna jambo wanahabari wamekuwa wakilikosa kwa muda sasa
ni kwanza kuwa na chombo kimoja kinachowaunganisha bila kuwabagua zaidi ya wao
tu kuwa wanahabari.
Katika
Baraza linaloanzishwa nimeona vifungu kuwa litakuwa na kazi nyingine muhimu na
ya kipekee (exclussive rights) ya kuandaa kanuni za maadili (media code of
ethics). Hii ni muhimu kwa sababu badala ya kutungiwa na watu wengine ni
wanahabari wenyewe watakaozitunga kwa sababu pia wanafahamu vyema kazi yao.
6.
Kamati ya
malalamiko
Kumekuwa
na fikra miongoni mwa watu kuwa kuipata haki mahakamani ni gharama kubwa sana
na inayochukua muda mrefu. Katikati ya keleleza za baadhi ya watu kuwa sheria
hii haina jema, ni muhimu kuona umuhimu wa kifungu hiki.
Kwa
kuanzishwa Kamati ya Malalamiko chini ya Baraza Huru la Habari, sasa wananchi
watapata pa kulalamikia na tena penye meno. Lazima tukubali kuwa ama kwa ajenda
fulani au makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari nchini vinawakosea sana watu
binafsi au taasisi.
Naamini
ni vyema kuwapa wahusika mahala pa kulalamika kwa sababu kwenda Mahakamani ni
suala ambalo kila mmoja, kwa sababu tulizokwishaeleza, asingependa kulichagua.
Kamati hii basi ikiundwa itoe uamuzi kwa haraka na iwe madhubuti.
7.
Bima ya
Afya
Mwezi
Novemba mwaka jana nilirejea nchini kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. Katika
pita pita zangu jijini Dar es Salaam nilikutana na matukio mawili ya wanahabari
kuchangiwa na wenzao.
Nilipofuatilia
suala hili nikaambiwa kuwa wanahabari hao hawakuwa na bima na walipopatwa na
maradhi ya muda mrefu ikawalazimu kuishi na kupata tiba kupitia michango ya
kujitolea ya wanataaluma wenzao.
Wapo pia waandishi
ambao hadi sasa wako hai lakini wanaishi kwa kutegemea misaada ya ndugu na
jamaa kwa ajili ya kupata huduma za afya. Nauona muswada huu unakuja kuwakomboa
wanahabari. Ni muswada unaokuja kuhakikisha kuwa si tu wanataaluma hii
wanafanya kazi zao kwa ufasaha lakini pia waweze kupata haki yao ya matibabu na
kuwekewa hifadhi ya jamii.
Iliniuma
na leo tunapoona katika kifungu cha 58 cha muswada huu kuna ulazima kwa
wamiliki wa vyombo vya habari kuwakatia bima watu wao, inashangaza kuona wapo
wanahabari ambao wanadai muswada huu haufai na kutaka urejeshwe nyuma.
8.
Haki za
watu
Ukisoma
Tamko la Haki za Binadamu la 1948 utaona msingi wa haki kuwa umebebwa katika
dhana ya haki ya mtu mmoja hukoma pale utekelezaji wa haki hiyo unapoingilia
uhuru au haki ya mtu mwingine.
Nimeviona
vifungu kadhaa vya muswada huu vikiwa na mlengo huu wa kuhakikisha wakati, kwa
mfano, haki ya wanahabari kukusanya na kusambaza habari ikiwa ni muhimu, pia
ziko haki za watu wengine zinazopaswa kulindwa na wanahabari.
Kifungu
cha 32 katika hili kwa mfano kinaainisha au kukataza waandishi kuchapisha kashifa
na kuwashushia watu wengine hadhi zao bila sababu (wawe hai au wamekufa). Hii
ni muhimu sana.
9.
Usalama wa Nchi
Nikikumbuka jinsi
vyombo vya habari vilivyochangia katika machafuko katika nchi mbalimbali
duniani hasa Rwanda (1994) na Kenya (2007) nashawishika kuchekelea ninapousoma
muswada huu.
Ukiacha vifungu
vinavyoainisha uchochezi, nimeguswa zaidi na kifungu cha 55 cha Sheria
kinapompa mamlaka Waziri akijiridhisha kuwa kuna suala linalokwenda kukiuka
usalama wa nchi basi achukue hatua haraka.
Wanaharakati hupinga
vifungu kama hivi kwa hoja za juu juu tu za kutokuwaamini viongozi wanaoweza
kupewa madaraka hayo, lakini uhalisi kwamba mambo haya yameshatokea na kwamba
zipo nchi zimeshawahi kuingia katika umwagaji wa damu kwa vyombo vya habari
kuachwa huru watakavyo, mtu hawezi kubeza kuwekwa kwa vifungu kama hivi.
Lipo pia kosa
la uchochezi ambalo wengi, bila kulitafakari, wanapiga kelele zilizokosa
tafakuri. Unawezaje kuwaacha watu watumie vyombo vya habari kuchochea vurugu,
kuhamaisha uasi na machafuko katika nchi? Kwangu mimi makosa kama haya ni muhimu
kwa usalama wa nchi na ni juu ya kila mmoja kutekeleza sheria.
10. Kufutwa
sheria ya Magazeti
Mimi nikiwa hapo
nyumbani kwa miaka mingi nimekisikia kilio cha wadau dhidi ya Sheria ya
Magazeti, 1976. Sheria hii tumekua nayo, tumeishi nayo na tulianza kuzeeka nayo
lakini kila mwanataaluma akijua haikuwa sheria nzuri.
Kwamba leo inafutwa
ni faraja kwa tasnia na nilidhani wenzetu wengine badala ya kulaani jambo hili wangeungana
nasi kulishangilia. Kwangu, kama kuna jambo jingine kubwa kwa wanatasnia
kulishangilia ni kufutwa kwa sheria hii ambayo wengine walifikia hatua ya
kuiita “ya kikatili.”
Wakati nikiamini
wabunge watakuwa wamefanyiakazi changamoto nyingine na kuuboresha muswada
katika maeneo machache kama vile kukamatwa mitambo kabla ya uamuzi wa mahakama
na kuainishwa viwango vya taaluma, niwaase wanahabri nchi kuwa katika ulimwengu
wa utatuzi wa migogoro; mazungumzo ni muhimu.
Ni bahati mbaya
kwamba katika hili walichagua kutozungumza na Kamati ya Bunge na wakasusia na
hatimaye muswada huu ukipita utawahusu hata kama wao hawakushiriki kuutunga.
*Mwandishi wa makala haya
amejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) kwenye Chuo
Kikuu cha Nottingham, Uingereza.
No comments:
Post a Comment