Na Mwandishi Wetu–Dodoma
Mkutano
wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeizuia Serikali
kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi Kati ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU) – (EPA) kwa
kuwa hauna manufaa kwa nchi ya Tanzania.
Uuamuzi huo
umetolewa leo mjini Dodoma na wabunge wa Bunge hilo baada ya kuujadili
mkataba huo kwa kina kwa kutoa maoni yao ambapo wengi wameunga mkono
kutosainiwa kwa mkataba huo.
Baadhi
ya wabunge waliopata nafasi ya kutoa maoni yao katika mjadala huo ni
pamoja na mbunge wa Mtwara Vijijini, Mhe. Hawa Ghasia ambaye amemshauri
Mhe. Rais Dkt .John Pombe Magufuli kutosaini mkataba huo kwa kuwa una
hasara nyingi kwa taifa kuliko faida.
”Kwa
kuzingatia mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru na
ukizingatia hakuna nchi hata moja ya Ulaya ambayo Tanzania inapeleka
bidhaa zake hivyo mkataba huu hauna maslahi kwa watanzania”, alisema
Mhe. Ghasia.
Aliongeza
kuwa Tanzania sio nchi ya kwanza kutosaini mkataba huo kwani kuna nchi
kama Angola, Nigeria, na Gambia hazijasaini,ameongeza kuwa kama Tanzania
itakubaliana na mkataba huo utaua viwanda pamoja na biashara za
Tanzania.
Kwa
upande wake Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Mhe.Hussein Bashe alisema kuwa
tatizo lililopo katika mkataba huo ni kutoitambua nchi kama nchi na
badala yake kuangalia nchi zote kwa pamoja hivyo amewashauri wabunge
kuhoji kuanzia kwenye kiini cha tatizo.
“Kwa
kuwa kifungu cha 143 cha mkataba huo kinaruhusu kupeleka marekebisho,
naishauri Serikali yetu ipeleke marekebisho ya kupendekeza kila nchi
iingie mkataba kivyake kulingana na maslahi ya nchi yake”, alisema
Bashe.
Aidha,
Mbunge wa Mwibara Mhe.Kangi Lugola (CCM) alimpongeza Mhe. Rais Magufuli
kwa kusita kusaini mkataba huo kwani ni miongoni mwa mikataba mibovu
kati ya mikataba iliyowahi kuletwa nchini kutoka katika nchi za Ulaya.
“Kama
tukikubali kusaini mkataba huu nchi hii itakuwa dampo la bidhaa
mbalimbali za ajabu kutoka nje na hivyo kupelekea kushindwa kutimiza
dhamira ya nchi ya kuimarisha viwanda vyetu”, alisema Mhe. Lugola.
Naye,
Mbunge wa Mchinga Mhe. Hamidu Bobali alisema kuwa mkataba huo haufai
kwa maslahi mapana ya taifa hili kwani unataka kuondoa ushuru kwa bidhaa
zinazoingia nchini wakati nchi ya Tanzania inaingiza bidhaa nyingi
kutoka nje kuliko kupeleka bidhaa nje ya nchi.
“Kama
tukikubali tukaondoa ushuru wa kuingiza bidhaa kutoka nje basi
tutapoteza mapato mengi yanayotokana na kuwepo kwa bandari pia
tunatakiwa tujiulize kama mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa
bidhaa huru je nchi yetu ina bidhaa zinazokidhi vigezo vya kuingia
katika nchi za Ulaya?” , alihoji Mhe. Bobali.
Mhe.
Bobali ametoa rai kwa Serikali kuileta Bungeni mikataba mikubwa kama ya
gesi na madini kwa ajili ya kujadiliwa kwa kina ili kuepuka kusaini
mikataba isiyo na tija kwa Taifa.
Baada
ya majadiliano hayo hatimaye Bunge limepitisha Azimio la
kuitaka Serikali kutosaini mkataba huo kwa sababu umeonekana kuwa na
mapungufu yanayohitaji marekebisho ambayo yataleta maslahi kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment